Timu ya Ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndugu Dominick Mbwete, leo Septemba 25, 2025, imeendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Katika kikao cha tathmini na wakuu wa idara pamoja na vitengo, Ndugu Mbwete aliwataka wataalamu kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha thamani ya fedha zinazotolewa na serikali inaonekana moja kwa moja kwenye ubora na matokeo ya miradi hiyo.
“Ni wajibu wetu, kama wataalamu, kuunga mkono jitihada za serikali kwa kuhakikisha kila mradi unaotekelezwa unaleta matokeo chanya kwa wananchi. Matokeo hayo yaweze kuonekana kwa kulinganisha fedha zilizotolewa na hadhi ya mradi husika,” alisema Mbwete.
Mbali na hilo, alisisitiza kuwa miradi iliyokamilika inapaswa kuanza kutoa huduma kwa wananchi, hatua ambayo itatimiza malengo ya serikali ya kusogeza huduma karibu na wanachi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Bi. Rehema Bwasi, aliahidi kushughulikia changamoto na dosari zilizojitokeza katika baadhi ya miradi. Aliongeza kuwa ofisi yake itaendelea kuwakumbusha wataalamu kutimiza majukumu yao ipasavyo ili kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo isikwame.
Ziara hiyo ilihusisha ukaguzi wa miradi 19 na kwa ujumla msisitizo mkubwa wa ziara hii ni kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo inakamilika kwa viwango vinavyokidhi thamani ya fedha za umma, sambamba na kutekeleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaletea wananchi huduma bora na endelevu.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.