


Ikiwa zimesalia siku chache kabla ya shule kufunguliwa nchini Tanzania leo Januari 06, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael Semindu, akiwa ameambatana na wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, amefanya ziara ya kutembelea miradi ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari.
Mhe. Semindu amesisitiza walimu kuhakikisha wanaandaa mazingira bora ya kujifunzia wanafunzi, ikiwemo kuzingatia usafi wa mazingira yote yanayozunguka shule.
“Ubora wa elimu unategemea mazingira ambayo wanafunzi wanajifunzia; tuendelee kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza elimu ya mazingira,” alisisitiza Mhe. Semindu.
Aidha, Mhe. Semindu amesisitiza miradi yote iliyopo katika hatua ya umaliziaji ikamilike kwa ajili ya mapokezi ya wanafunzi.
Naye Kaimu Mkurugenzi, Dkt. Adrianus Kalekezi, ameahidi kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha mazingira yote ya shule yanakuwa safi ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi wawapo katika maeneo ya shule.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.