
WASIMAMIZI WA VITUO NA WASAIDIZI WAO WASISITIZWA KUVIISHI VIAPO
Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Mbulu Mjini, Ndugu Joseph Geheri, ametoa rai kwa Wasimamizi wa Vituo na Wasimamizi Wasaidizi kuhakikisha wanaishi kwa vitendo viapo vyao vya kazi katika kipindi chote cha uchaguzi.
Geheri alitoa kauli hiyo akimuwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Ndugu Philemon Maffa, wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili (02) kwa Wasimamizi wa Vituo na Wasaidizi wao. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Akizungumza na washiriki, Ndugu Geheri aliwataka Wasimamizi hao kwenda kutekeleza majukumu yao kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa uadilifu na uwajibikaji.
“Niwakumbushe kuviishi viapo vyetu vya kutunza siri, kufanya kazi kwa uzalendo, na kushirikiana kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu,” alisema Ndugu Geheri.
Aidha, aliwakumbusha washiriki kuzingatia muda wa kufungua na kufunga vituo siku ya uchaguzi, akibainisha kuwa vituo vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
Kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Ndugu Lawrence Tsino alitoa shukrani kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwapatia mafunzo yenye manufaa kuelekea uchaguzi huo.
Uchaguzi Mkuu wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano, Oktoba 29, 2025.
“KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA.”b
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.