Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mhe. Michael Semindu, amewasisitiza wananchi wa Kitongoji cha Tipri kuendelea kutunza miundombinu ambayo serikali imeendelea kuiboresha kwaajili ya maslahi ya wananchi.
Rai hii imetolewa leo Julai 10,2025 akiwa katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Daraja la Kamba la watembea kwa miguu katika Kijiji cha Tsawa na kitongoji Tipri.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe.Semindu amewasisitiza wananchi kuwa mstari wa mbele kutunza na kulinda miradi ili kuendelea kuwa na tija kwa wananchi wote na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Tuendelee kuunga mkono jitihada za serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwani miradi mingi inaletwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote", alisema Mhe.Semindu
Sambamba na hayo Mhe.Semindu amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu siku ya Jumatano tarehe 16/ 07/2025.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Tsawa, Mhe.Sisirini Malley, ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutatua changamoto iliyokuwa inawatesa wananchi wa Kitongoji cha Tipri hasa kipindi cha masika ambapo mawasiliano yalikuwa yanakatika.
Mradi wa Daraja la Kamba la watembea kwa miguu linatarajiwa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2025.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.