TIMU YA WATAALAMU(CMT) YAFANYA ZIARA YA KUTEMBELEA MIRADI
Posted on: October 18th, 2025
TIMU YA WATAALAMU (CMT) YATEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO MBULU MJINI
Timu ya Wataalamu ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu (CMT) ikiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Bi. Rehema Bwasi, tarehe Oktoba 18, 2025, imefanya ziara ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya halmashauri.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Rehema amewataka mafundi na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuanza kutumika kwa manufaa ya wananchi.
“Niwatake wakandarasi wote kuhakikisha kazi mlizopewa zinakamilika kwa wakati. Ikitokea changamoto yoyote, iwasilishe kwa wataalamu wetu mapema ili ipatiwe ufumbuzi bila kukwamisha utekelezaji wa mradi,” alisema Bi. Rehema.
Aidha, aliwataka wahusika wote kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana katika maeneo ya miradi muda wote, ili kuepusha ucheleweshaji wa kazi kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu.
Miradi iliyotembelewa na timu hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kituo Kipya cha Afya cha Murray,Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Uzio wa Bweni la Wasichana Wenye Mahitaji Maalumu Endagkot, na Jengo Jipya la Utawala.