
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amewasihi Watanzania kuendelea kudumisha na kulinda amani iliyopo nchini kwa nguvu zote.
Dkt. Mpango alitoa wito huo Oktoba 14, 2025, jijini Mbeya, wakati akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025, ambapo mwenge huo umekimbizwa katika Halmashauri 195 za Tanzania Bara na Visiwani.
“Mwenge wa Uhuru ni tunu muhimu kwa Taifa letu. Tunapaswa kuwafundisha watoto wetu kuhusu historia yake na mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika kuasisi Mwenge huu,” alisema Dkt. Mpango.
Amesisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya Taifa, hivyo Watanzania wanapaswa kuendelea kuishi kwa upendo, mshikamano na bila ubaguzi wa aina yoyote.
“Tukumbuke kuwa amani ni urithi wetu wa thamani. Tuihifadhi, tuitunze, na tuhakikishe tunaendelea kuishi kwa umoja kama Watanzania,” aliongeza.

Wakati huohuo, Makamu wa Rais amewakumbusha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kote nchini.

Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.