Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi huduma ya kusafisha damu (Dialysis) pamoja na huduma ya kipimo cha mfumo wa chakula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, hatua hiyo inayolenga kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe.Sendiga ameeleza kuwa mpango huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya na kuzisogeza karibu na wananchi.
“Huduma hii ni ya kisasa na muhimu sana kwa wakati huu, hasa ikizingatiwa kuwa magonjwa ya figo yanaongezeka kwa kasi duniani,” alisema Mhe. Sendiga.
Awali, wagonjwa waliokuwa wakihitaji huduma za kusafisha damu walilazimika kwenda Hospitali ya Rufaa ya Haydom au hospitali nyingine zilizoko mbali, jambo lililoongeza gharama na usumbufu mkubwa kwao na familia zao. Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana mkoani Manyara, na hivyo kuondoa adha ya kusafiri umbali mrefu.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.