Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbulu Bi. Rehema Bwasi amewaasa wananchi wa Mji wa Mbulu kujitokeza kuomba mikopo iliyotengwa kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Bi. Rehema ametoa rai hiyo mapema leo Jumapili tarehe 6 Oktoba 2024 akizungumza na Wananchi kupitia Redio Habari Njema 87.5 Mhz ambapo amesema kiasi cha Shilingi Milioni 186,000,000/= zimetengwa kwa kipindi cha robo ya pili mwaka wa fedha 2024/2025.
"Kwanza nimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha mikopo hii muhimu kwa watanzania ambao hawana kazi rasmi, hii ni fursa kubwa sana kwa Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu"
"Niwasihi makundi tajwa tujitokeze kwani sasahivi tunaendelea na mafunzo kwa Kamati mbalimbali za mikopo ikiwemo zile za Kata, Wilaya na wataalamu kama Watendaji na maafisa Maendeleo hivyo mjitokeze kwa wingi kupitia vikundi ili muweze kupata mikopo hii"
Vikundi vinavyotakiwa kuomba mikopo vinapaswa kuwa na sifa zifuatazo:-
1. Kikundi cha Wanawake, vijana na wenye ulemavu kilichotambuliwa na kupewa cheti cha utambuzi na Halmashauri
2. Kikundi kiwe kinajishughulisha na shughuli za ujasiriamali mdogo, wa kati au kinachotarajia kuanzisha shughuli za ujasiriamali
3. Kikundi cha Wanawake na Vijana kiwe na Idadi watu wasiopungua watano na Kikundi cha watu wenye ulemavu wasipungue wawili
4. Kikundi kiwe na Account Benki iliyofunguliwa kwa jina la kikundi husika
5. Wanakikundi wawe raia wa Tanzania waio na ajira rasmi na wawe na miaka kuanzia 18 hadi 45
Maombi yote yatumwe kupitia mfumo wa kielektorniki (tembelea tovuti: mikopohalmashauri.tamisemi.go.tz) ili kutambuliwa na kuomba mkopo au wasiliana na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata husika au mtendaji wa Kata husika.
Vilevile kikundi kinapaswa kuwa na barua ya kikundi ya kuomba mkopo iliyopotishwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji/Mtaa, muhtasari wa Kikundi wa kuomba mkopo na andiko rahisi la mradi
Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 20 Oktoba, 2024
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.