Wenyeviti wa mitaa na Vitongoji, pamoja na Wajumbe Halmashauri za Mitaa, Vijiji na vitongoji kundi Mchanganyiko na Viti Maalumu Wanawake( Wateule) , wameapishwa leo Novemba 28, 2024, katika maeneo tofauti Halmashauri ya Mji wa Mbulu, mara baada ya kukamilika kwa zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na vitongoji ambao umefanyika jana Novemba 27,2024.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi.Rehema Bwasi,amewataka viongozi wapya ngazi za mitaa, Vijiji na Vitongoji kuhakikisha kuwa wanatenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao, mara baada ya kuaminiwa na wananchi kupitia Uchaguzi huo ambao umefanyika tarehe 27/11/2024.
“Nendeni mkafanye kazi Kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo katika maeneo yenu huku tukizingatia 4R za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.Alisema Bi.Rehema
Bi.Rehema amesema hayo, leo Novemba 28, 2024, wakati wa zoezi la kuapishwa kwa Viongozi ambao ni Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji kundi Mchanganyiko pamoja na Wanawake Viti Maalumu.
Zoezi hilo la uapisho wa Viongozi hao limeongozwa na Mhe. Hakimu Mkazi Mwandamizi Johari Hamid Kijuwile ,Mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Bi.Rehema Bwasi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 umekuwa na Kauli mbiu isemayo Serikali za Mitaa Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki uchaguzi.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.