WALIMU WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO SHULENI
Ili kuimarisha ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo shuleni Septemba 26,2025 Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeendesha mafunzo elekezi kwa Walimu mafunzo ambayo yalienda sambamba na hafla ya pongezi kwa shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya wanafunzi.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Walimu kuhusu usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa shuleni, hususan katika maeneo ya manunuzi, ujenzi na ukaguzi, ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha za umma.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Bi. Marcelina Saura, amewataka walimu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma (PPRA) wakati wa utekelezaji wa miradi, akisisitiza kuwa ufuataji wa taratibu hizo ni nguzo muhimu ya uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za serikali.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Halmashauri, Ndugu Andrew Magesa, amehimiza ushirikishwaji wa kamati husika katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ili kuongeza uwazi na umiliki wa jamii. Ameongeza kuwa ni muhimu vifaa vyote vya ujenzi vikaguliwe na wataalamu kabla ya matumizi, ili kuepuka upotevu wa rasilimali na kuhakikisha ubora wa miundombinu inayojengwa.
Naye Mkaguzi wa Ndani, Bi. Tumaini Mwangatwa, amekumbusha Walimu kuwa wanapaswa kusimamia kikamilifu miradi wanayopewa dhamana ya kuitekeleza, kuhakikisha kuwa thamani ya mradi inaendana na fedha zilizotolewa na serikali, hatua itakayosaidia kujenga imani ya wananchi na kuimarisha uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma.
Akihitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Bi. Rehema Bwasi, amewapongeza Walimu kwa mafanikio waliyopata katika sekta ya elimu na kuwasisitiza kutumia elimu waliyoipata kwenye mafunzo hayo katika kusimamia miradi kwa weledi, ubunifu na uadilifu, ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora unaoendana na viwango vya serikali.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.