Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu wametakiwa kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya rushwa kwa kuelimisha jamii na kuzingatia maadili ya uadilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mashuleni.
Wito huo umetolewa leo Septemba 26, 2025, na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mbulu, Ndugu Lawrence Mlaponi, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu kwa ufaulu mzuri wa wanafunzi kwa mwaka 2024.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ndugu Mlaponi alisema rushwa imeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika kufanikisha miradi ya maendeleo, hivyo walimu wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na kuwa mfano wa kuigwa katika kuzuia vitendo hivyo.
“Nendeni mkawe mabalozi wa mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwaelimisha wengine kuhusu madhara yake. Kumbukeni, rushwa inasababisha serikali kushindwa kufikia malengo yake ya kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Ndugu Mlaponi.
Aidha, alisisitiza kuwa miradi yote ya maendeleo inapaswa kusimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora unaostahili na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.
“Wataalamu wa sekta mbalimbali wanapaswa kufuatilia kwa ukaribu miradi inayoendelea ili kuhakikisha ubora unazingatiwa kulingana na miongozo na taratibu zilizowekwa,” aliongeza Mlaponi.
Sambamba na hayo, amekumbusha umuhimu wa kuzingatia misingi ya ushirikishwaji wa wananchi, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi, akibainisha kuwa ushiriki wa jamii ni nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi inakuwa endelevu na yenye manufaa kwa wananchi wote.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.