Wafanyabiashara Halmashauri ya Mji wa Mbulu wameshauriwa kutojihusisha na ukopaji wa mikopo kausha damu isiyozingatia vigezo na kupelekea kushindwa kujiinua kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya mji wa Mbulu Bi.Anamary wakati wa utoaji wa Elimu ya uendeshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara na wajasiriamali iliyofanyika leo tarehe 13 Disemba, 2024 Mjini Mbulu.
Bi.Anamary amesema kumekuwa na Wafanyabiashara na wajasiriamali wanaokopa fedha katuka taasisi bubu (Zisizotambulika) au kwa watu binafsi na kupelekea kulipa mikopo kwa gharama kubwa au kunyang’anywa vitu vyao jambo linalohatarisha uchumi wao na kushindwa kukua kibiashara.
“Tuachane na hii mikopo kausha damu ambayo inawatesa wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wafanyabiashara na wajasiriamali wa hapa Mbulu, tujiunge vikundi au kufungua akaunti kwenye Mabenki ili tuwe na sifa za kukopeshwa kwa gharama nafuu”.Alisema Bi.Anamary
Kwa upande wake Afisa Biashara Halmashauri ya mji wa Mbulu Ndugu.Zabron Marwa amesema Wafanyabiashara wanapaswa kufuata taratibu za ufanyaji wa Biashara na kuwa na Leseni za kutoa huduma hizo ikiwemo kufuata taratibu zote za kulipia Leseni za biashara kwa wakati.
“Tufanye biashara kwa kuzingatia miongozo na Sheria zilizowekwa kwa mujibu wa Nchi yetu na tulipie leseni kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza”.Alisema Ndugu Marwa
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.