Kamati ya Fedha Halmashauri ya Mji wa Mbulu imewataka walimu na wazazi kushirikiana ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari Wilayani Mbulu.
Rai hiyo imetolewa leo Februali 10,2025 na Kamati ya Fedha inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mhe. Peter Sulle wakiwa katika ukaguzi wa miradi ya Maendeleo hususani Madarasa, vyoo na Mabweni yanayojengwa katika shule ya Sekondari Gehandu, Ayamohe na Chief Sarwatt.
Kamati hiyo imesema, Serikali ya awamu ya 6 imeendelea kujenga miundombinu kwenye shule mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma na kuishi katika mazingira rafiki hivyo jukumu la Wazazi na walimu ni kushirikiana ili wanafunzi waweze kusoma na kufaulu vizuri katika masomo yao.
Vilevile Kamati hiyo imeshauri usimamizi wa karibu kwenye miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati kwa kuwa lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona fedha zilizotolewa zinatekeleza miradi hiyo kwa ubora unaostahili na wakati muafaka.
Wakati huohuo, Kamati hiyo imewashukuru wananchi wa Halmashauri wa Mji wa Mbulu kwa ushirikiano wanaoutoa katika utekelezaji wa miradi hiyo pale nguvu na muda wao unapohitajika ili kusaidia utekelezaji wa miradi hiyo kutokuwa mgumu.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.