


Wananchi wa Kijiji cha Tsaayo wamehimizwa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote kama hatua ya mapema ya kujikinga na changamoto za kiafya na kulinda uchumi wa familia zao.
Rai hiyo imetolewa leo, Februari 17, 2026, wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya bima ya afya lililofanyika kijijini hapo, likiwalenga makundi mbalimbali ya jamii.
Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa Bima ya Afya, Dkt. Basil Manda, amesema kujiunga mapema na bima ya afya kunapunguza athari za kifedha zinazotokana na magonjwa ya ghafla na ni kinga muhimu ya maisha.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha huduma za afya na kusogeza huduma karibu na wananchi, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kujiunga na bima.
Dkt. Manda amesisitiza kuwa mpango huo una faida nyingi ikiwemo kupata huduma katika vituo vilivyosajiliwa, kupunguza ucheleweshaji wa matibabu na kuongeza uhakika wa huduma kwa familia.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Ndugu Tomic Simbeye, amesema afya bora ni msingi wa maendeleo na kujiunga na bima ni njia ya kujilinda dhidi ya gharama zisizotarajiwa za matibabu.
Amehimiza wazazi kuhakikisha wanawaandikisha watoto wao ili kulinda ustawi wa familia na mustakabali wao wa kiafya.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Tsaayo, Ndugu Silvin Bura, amewashukuru wataalamu kwa kutoa elimu hiyo na kuhimiza wananchi kujiunga kwa wingi na mpango wa bima ya afya.
Wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali na kupewa ufafanuzi kuhusu taratibu za kujiunga, uchangiaji na matumizi ya huduma za bima.
Utoaji wa elimu ya bima ya afya unaendelea katika maeneo mbalimbali ili kuongeza usajili wa wananchi na kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.