Viongozi wa dini wilayani Mbulu wamewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kuepuka uvunjifu wa amani.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 24, 2025, wakati wa maombezi maalum yaliyofanyika kwa ajili ya kuombea taifa na kuombea Uchaguzi Mkuu kupita kwa amani na utulivu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Wilaya ya Mbulu, Mchungaji Augustino Halule, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, akisisitiza kuwa kushiriki uchaguzi ni njia muhimu ya kulinda na kudumisha amani.
“Ni wajibu wetu kuilinda amani ya Tanzania, hivyo twende tukawachague viongozi tunaowataka kwa ajili ya maendeleo yetu wenyewe,” alisema Mchungaji Halule.
Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti Mkuu wa Mbulu, Hassan Abubakari, amewakumbusha wananchi kuzingatia sera na ahadi za wagombea badala ili kuepuka migongano na misuguano katika uchaguzi mwingine.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Ndugu Paulo Bura, amewataka washiriki na waumini kuendelea kuwa chachu ya amani kwa kuwahamasisha wananchi wengine kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni haki ya msingi na ya kikatiba ya kila Mtanzania.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.