“Tutahakikisha tunakabiliana na matukio ya ukatili yanayowasibu wanafunzi wawapo shuleni na nyumbani ili kuwa na Jamii yenye haki na usawa”
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi. Rehema Bwasi akiwa na Maafisa Elimu Kata, Maafisa Ustawi wa Jamii na Walimu wakuu Shule za Sekondari mapema leo tarehe 7 Aprili, 2025 baada ya kuitisha kikao kilichojadili namna ya kuweka Ulinzi na Usalama wa mtoto.
Bi. Rehema amesema ni lazima Walimu na wazazi kushirikiana kikamilifu ili kuwatetea watoto waweze kufikia ndoto zao kwa kuweka mipango mikakati ya kuwasaidia watoto wanapokuwa Shuleni na nyumbani.
Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Mbulu Bi. Saada Kabyemela amesema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Walimu kwa kufuatilia mienendo ya watoto katika mazingira yao ya kujisomea na kuifundisha jamii mbinu za kuripoti matukio ya ukatili kwa watoto ili kuondokana na wimbi la unyanyasaji kwa watoto.
Kwa upande wake Afisa ustawi wa Jamii Ndugu. Tomic Simbeye amewasihi walimu kuendelea kushirikiana kutoa taarifa kwa wakati kuhusu matukio yote yanayowahusu watoto ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa haraka.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.