TAREHE 17 JANUARI,2025 WANAFUNZI WAWE WAMERIPOTI SHULE-DC KESSY
Posted on: January 15th, 2025
Wazazi na walezi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shule wameagizwa kuhakikisha ifikapo tarehe 17 Januari, 2025 wanafunzi wote wawe wamesharipoti shuleni na kuanza masomo.
Maagizo hayo yametolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Veronica Kessy akiwa ziarani kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
"Maelezo haya lazima yasimamiwe wazazi na walezi wote ambao wanafunzi wao hawajaripoti shuleni tangu Jumatatu, wahakikishe mpaka kufikia mwishoni mwa wiki hii tarehe 17 Januari, 2025 wanafunzi wote wawe shuleni na kuanza masomo yao mara moja, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao".Alisema Mhe.Kessy
Mhe. Kessy ameongeza kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kujenga miundombinu ya Elimu, hivyo hataki kuona mwanafunzi ameshindwa kusoma kwa sababu ya kukosa sare za shule au kitu chochote bali waanze masomo wakati walezi wakishughulikia jambo hilo.
Amewasisitiza Walimu kuweka mikakati ya ufaulu kwa wanafunzi na kuwafundisha kwa bidii na uzalendo kama watoto wao ili kusaidia juhudi za Mhe. Rais kupambana na ujinga kwa wanafunzi na kuinua viwango vya taaluma nchini.
"Ni matarajio ya Serikali kwa namna ambavyo Mhe. Rais anavyoboresha miundombinu wazazi na walimu mtatoa ushirikiano kuhakikisha watoto wetu wanasoma na kufaulu vizuri katika masomo yao" Alisema Mhe. Kessy