Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Ndugu Faraja Ngerageza, ametoa rai kwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi ya maendeleo viporo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto leo Desemba 03, 2025, Ndugu Faraja amesema madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika haraka ili kutimiza matakwa ya Serikali ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Aidha, Ndugu Faraja aliwasihi kushirikiana na viongozi na wataalamu ili kuhakikisha mapato ya Halmashauri yanakusanywa ipasavyo huku akiwakumbusha kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Awali, Mwenyekiti wa Muda wa kikao hicho, Ndugu Paulo Bura, wakati akifungua mkutano huo aliwataka madiwani kutimiza ahadi walizowapa wananchi wakati wa kampeni na kuwatumikia kwa weledi.
Vilevile aliwahimiza madiwani hao kusoma na kufahamu miongozo ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Ndugu Bura amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na viongozi wengine ni msingi muhimu wa kufanya baraza kuwa na nguvu na uwezo wa kupanua wigo wa mapato ya Halmashauri.


Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.