Wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya Afya na Elimu Wilayani Mbulu wameagizwa kukamilisha miradi yao kwa wakati ili kutimiza malengo ya Serikali kwa wakati.
Maagizo hayo yametolewa leo Januari 13, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Veronica Kessy akiwa katika ukaguzi wa miradi hiyo Kata ya Tlawi, Imboru, Endagkot na Sanubaray baada ya kushuhudia kusuasua kwa baadhi ya miradi.
"Nataka miradi yote ikamilike kwa wakati ili ianze kutumika kama Serikali ilivyokusudia kusogeza huduma karibu na mwananchi, sasa inaposuasua kukamilika kwake itasababisha kutofikisha huduma kwa wakati kama inavyotarajiwa na Serikali kwa kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kujenga Hospitali, Vituo vya Afya, madarasa na huduma nyingine nyingi ili wananchi wasifuate huduma hizo umbali mrefu" amesisitiza Mhe. Kessy
Wakati huohuo Mkuu wa Wilaya ameendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi kupeleka wanafunzi shuleni kwani shule tayari zimefunguliwa na masomo yameanza.
"Niwasihi wazazi na walezi tupeleke watoto wetu wakasome kwani miundombinu yote muhimu imeshakamilika na fedha nyingi zimeletwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu hapa Wilayani kwetu, hivyo tuhakikishe watoto wetu wanakwenda shuleni" Aliongeza Mhe. Kessy
Mhe. Kessy anaendelea na ziara ya siku tatu kuanzia leo tarehe 13 Januari hadi tarehe 15 Januari, 2025 kukagua miradi kwenye Kata mbalimbali za Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Picha mbalimbali zikionesha baadhi ya miradi iliyokaguliwa leo na maendeleo yake
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.