NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefunga rasmi maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kaskazini katika viwanja vya Taso Themi Jijini Arusha.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maonesho hayo Ulega amesema kuwa amefurahishwa na Paredi ya Mifugo aliyoiona katika paredi ya mifugo na kuupongeza mkoa wa Arusha kwa kuwa wafugaji wenye mifugo bora tofauti na alivyodhani.
Amesema katika maonesho hayo amezoea kuona mifugo bora inatoka kwa Taasisi za Serikalini kama Ranchi ya Taifa (NARCO), Jeshi la Magereza lakini wafugaji kutoka wilaya za Monduli, Longido, Ngorongoro ndio wameibuka Vinara wa kuwa na Mifugo bora.
Hata hivyo amezitaka Taasisi mbali mbali viwanjani hapo kutoa taarifa za vipeperushi kwa wakulima na wafugaji tofauti na maelezo ili kuwawezesha, wakulima na wafugaji kutunza kumbukumbu na kufanya rejea hapo baadae kwa kuwa hawawezi kukumbuka kila kitu.
Ulega amesema amefurahishwa na Tasisi za fedha ambazo zimeonesha kuwasaidia wakulima na wafugaji viwanjani hapo kwa kutoa mikopo ya mitaji kwa kuwa ni changamoto ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu sasa.
Amesema Serikali itafurahishwa endapo itaona uwekezaji mkubwa wa viwanda vya kusindika mazao ya Kilimo na kuchakata Mifugo, kwa kuwa mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha uwepo wa rasilimali ni mkubwa.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.