MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Mbulu wakiongozwa na DC wao Chelestino Simbalimile Mofuga kwa namna wanavyowatumikia wananchi hadi kupunguza kero kila mahali anapopita kwenye mikutano yake anakutana na changamoto chache.
Mnyeti akizungumza na wananchi wa Mbulu mjini amesema viongozi wa wilaya hiyo wamejitahidi kupunguza kero za maeneo inayowazunguka hadi yeye wanampunguzia kazi katika eneo hilo.
“Jana nilipita Kainam na kuzungumza na wananchi baada ya kukagua mabweni ya wasichana kwenye shule ya sekondari kisha nikaenda Hhaynu nikaweka jiwe la msingi la shule ya sekondari na kuzungumza na wananchi ambapo watu wawili walijitokeza kutoa kero,” alisema Mnyeti.
Alisema watu hao walizungumzia barabara na umeme hivyo kudhihirisha kuwa viongozi wa Mbulu wanawatembelea wananchi na kusikiliza kero zao.
“Nimefika Tlawi jana na leo nimekwenda Qatesh, Titiwi, Gehandu na Gedamar huko kero za wananchi ni chache na hapa Mbulu mjini watu watatu wamejitokeza kutoa kero hapa mmeonyesha kazi imefanyika,” alisema Mnyeti.
Aliwapongeza Mofuga, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Sarah Sanga, Mkurugenzi wa Mji wa Mbulu Anna Mbogo na viongozi wengine wa eneo hilo kwa kutatua migogoro, kero na changamoto za wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu Mofuga alishukuru kwa hatua hiyo ya kutambuliwa kazi nzuri wanayofanya kwani kila alhamisi wametenga kukutana na wananchi wenye matatizo ofisini kwake na pia kuwatembelea kwenye maeneo yao.
“Tutahakikisha jamii inasaidiwa kwenye kutatuliwa kero zao ili kuhakikisha wananchi wanaipenda serikali yao inayoongozwa na Rais John Magufuli,” alisema Mofuga.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.