Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kupunguza umasikini kwa Wananchi wake kupitia utoaji wa mikopo isiyo na riba.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo tarehe 7 Februali, 2025 Jijini Dodoma baada ya kushuhudia hafla ya utiaji saini wa mikopo ya 10% kati ya Halmashauri kumi (10) ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Mabenki.
Benki zilizoingia makubaliano na Halmashauri ni NMB, CRDB, UCHUMI COMMERCIAL BANK ambapo Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha vikundi vinapata mikopo isiyokuwa na riba na kufuatilia matokeo ya mikopo hiyo ili iwe na tija katika ukuaji wa uchumi kwa Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Mhe. Peter Sulle, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi. Rehema Bwasi na wataalamu mbalimbali wameshuhudia hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Halmashauri ya Mji wa Mbulu imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 186 kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.