


Desemba 04, 2025, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu, Ndugu Paulo Bura, amefungua mafunzo ya madiwani yenye lengo la kuwajengea uwezo juu ya utendaji kazi katika kipindi cha miaka mitano (2025–2030).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Ndugu Bura amewasisitiza madiwani kuzingatia maadili ya viongozi wa umma, huku akiwaasa kuendelea kutii sheria, kanuni na taratibu za Halmashauri ili kuboresha utendaji kazi.
Naye, Afisa Maadili, Ndugu Adam Kuhanda, amewaeleza madiwani juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili katika utumishi wa umma.
“Ubora katika utendaji kazi uende sambamba na kujiheshimu huku mkizingatia maadili ya uongozi katika maisha ya kila siku,” alisema Bw. Kuhanda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mbulu, Ndugu Lawrence Mlaponi, amewasisitiza madiwani kujiepusha na vitendo vya rushwa katika maeneo yote na kuepuka kutoa rushwa, jambo ambalo linaweza kuwaweka matatani ilihali wanajua kuwa rushwa ni adui wa haki na si kitendo cha uungwana katika uadilifu.
Maafisa Mipango pamoja na wakuu wa idara mbalimbali wameomba ushirikiano kamili kutoka kwa Waheshimiwa Madiwani katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao, ili kuhakikisha miradi hiyo inapelekwa stahiki kwa wananchi na kukamilika kwa wakati.
Kwa niaba ya madiwani wote, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Sylvester Ombay, ameshukuru kwa elimu iliyotolewa na kueleza kuwa itakuwa msaada mkubwa katika kuboresha utendaji kazi.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.