Maafisa Habari Nchini wameaswa kutoa habari na taarifa sahihi kwa Jamii inayowazunguka kwa wakati ili kuwa na Jamii inayoelewa masuala yanayohusu maendeleo yanayofanyika Nchini
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe Mohamed O. Mchengerwa(Mb) Leo Mei 23, 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi za Ofisi ya Rais TAMISEMI katika Ukumbi wa Mikutano Dodoma Jiji ulipo Mji wa Serikali Mtumba.
Katika Kikao Kazi hicho Mhe. Mchengerwa amewataka Maafisa Habari Nchini kutoa taarifa sahihi ya yale yanaoyoendelea kwenye maeneo yao.
“ Ninyi ni nguzo ya maamuzi ya kuwalisha watanzania ya kile kinachoendelea katika maeneo yenu kwani Maafisa Habari mnayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki yao ya msingi ya kupata taarifa sahihi na kwa wakati.” Amesema Mhe Mchengerwa.
Aidha amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI ni Wizara inayobeba karibu 21% ya Bajeti Kuu ya Serikali ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Ofisi ya Rais TAMISEMI imepitishiwa bajeti ya Shilingi 11,782,984,202,000.00 ambazo zinakwenda kutekeleza miradi kwenye Taasisi, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Pamoja na hayo Mhe Mchengerwa amewataka Maafisa Habari kuweka Uzalendo mbele katika kuisemea miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika maeneo yao kwani fedha nyingi za maendeleo zinapelekwa huko ili kuboresha huduma za Afya, Miundombinu ya Barabara, Elimu, Umeme, Mawasiliano, n.k
Kikao hicho kitafanyika kwa siku mbili ambapo Maafisa Habari kote Nchini wamekutana kuendelea kubadilishana uzoefu namna bora ya kuzitangaza kazi za Serikali katika maeneo yao.
Miongoni mwa Halmashauri zilizoshiriki Kikao Kazi hicho kutoka Mkoa wa Manyara ni pamoja na Halmashauri ya Mji wa mbulu, Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Kiteto, Babati na Hanang.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.