Kamati za Ujenzi na wasimamizi wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Halmashauri ya Mji wa Mbulu wametakiwa kusimamia fedha hizo kwa umakini ili kutekeleza miradi husika.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Veronica Kessy mbele ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi. Rehema Bwasi, Katibu Tawala Wilaya Ndugu. Paulo Bura ,wataalamu mbalimbali na viongozi wa Kamati za miradi akiwa kwenye ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo tarehe 14 Januari, 2025.
Mhe. Kessy amesema Serikali imeleta fedha nyingi kutekeleza miradi ambayo lazima isimamiwe kikamilifu na isipotee au kutumika tofauti na kusudio husika.
"Lazima fedha hizi zifanye kazi iliyolengwa, niwasihi Viongozi, Wataalamu na wanakamati mnaohusika kwenye usimamizi wa miradi hii fedha zifanye kazi husika na si vinginevyo".Alisema Mhe.Kessy
Aidha, amesisitiza wananchi kushiriki katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ili kuunga mkono Jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ziara ya Mkuu wa Wilaya imefanyika leo katika kata ya Nambis, Murray, Nahasey na Kainam ambapo hapo kesho ataendea na ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi katika kata zingine.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.