Serikali imezitaka Halmashauri zote nchini kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya kuupokea mfumo ulioboreshwa wa usimamizi na uendeshaji wa shughuli za afya (Improved Government of Tanzania Health Operations Management Information System-GoTHOMIS), unaomaliziwa kusukwa hivi sasa na wataalamu wazawa.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima, muda mfupi baada yakutembelea kikosi kazi hicho mkoani Morogoro kinachoiendelea na kazi ya usukaji wa mfumo.
Akizungumza mara baada yakupata wasilisho kutoka kwa wataalam, Dkt. Gwajima, alisema Serikali imejizatiti katika uimarishaji wa miundombinu ya afya lakini uimarishaji huo wa miundombinu utakuwa na maana sana kama mifumo madhubuti na yenye tija itasimikwa katika kila kituo cha kutolea huduma za afya.
“Nakosa cha kuongea maana nimezunguka nchi hii takribanini yote sasa, matatizo makubwa yaliopo huko, ni pamoja na utunzaji mbovu wa kumbukumbu, hivyo tukiwa na mfumo kama huu ni matumaini yangu tutakuwa tumepata suluhu ya kudumu” alisema Dkt. Gwajima, na kuongeza kuwa “kwa kuwa kipindi hiki ni cha maandalizi ya bajeti kila kituo kione uwezekano wakutenga milioni 10 kwa ajili ya vifaa. Aidha kwa upande wa zahanati wanaweza kuwatumia wadau na nimelichukua tuone tutalishughulikiaje” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Awali akitoa wasilisho kwa niaba ya kikosi kazi, mtaalam wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Melkiory Baltazari alisema kwamba, mara baada ya kukamilika kwa mfumo yatahitajika mafunzo kwa watumiaji wa mfumo kwani maboresho yaliyofanyika ni muhimu mtumiaji kupata kuujua mfumo.
“Mhe. Naibu Katibu Mkuu, tunajua kwa sasa hatuna kada ya watu wa TEHAMA kwenye ngazi ya kituo, hivyo tunategemea kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huu ili waweze kuutumia kikamilifu mara baada ya maboresho haya” alifafanua Melkiory.
Mapema tarehe 10 na 11 Novemba, 2019, kikosi kazi hicho kilipokea ugeni wa Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa nyakati tofauti ambapo katika maelekezo yote, walikitaka kikosi kazi kukamilisha kazi nifikapo tarehe 30 Machi, 2020.
Mapema akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu kuzungumza na kikosi kazi, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Erick Kitali, alisema kazi hiyo itakamilika kwa wakati na mara baada yakukamilisha kazi mfumo huo utasimikwa kwenye vituo vyote vya kutoa huduma za afya vilivyopangwa.
“Ndugu Naibu Katibu Mkuu, pamoja na kwamba tulipanga kazi hii ikamilike mwezi Machi na kwa muelekeo ulivyo tumefikia asilimia 70, hata hivyo tupo tayari kupokea maelekezo yako” alisema Kitali
GoTHOMIS Iliyoboreshwa ni mfumo muendelezo wa GoTHOMIS ya mwanzo ambayo ilifungwa na kuonesha mafanikio makubwa kuanzia ngazi ya Vituo vya Afya mpaka Hospitali za Mikoa na tayari zaidi vituo 518 yalikuwa yamefungiwa mfumo huo kusadia hasa katika suala zima la utoaji wa huduma bora, utunzaji wa kumbukumbu, kuongeza ufanisi wa kazi na kudhibiti mapato ya serikali yaliyokuwa yakipotelea mikononi mwa watu waovu wachache.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.