Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga leo Januari 29, 2025 amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael John Semindu kuwa Mkuu wa wilaya ya Mbulu baada ya kuteuliwa na Mhe.Rais tarehe 25 Januari,2025.

Hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara mjini Babati, na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya siasa.
Akizungumza na Wakuu wa Wilaya mara baada ya uapisho Mkuu Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga alitoa pongezi kwa Mkuu wa Wilaya mpya na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza nguvu kazi ya watendaji katika Mkoa wa Manyara.
Aidha, Mhe. Sendiga aliwaelekeza Wakuu wa Wilaya hao vipaumbele vyake katika utendaji wa kazi ikiwemo; ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuwahudumia Wananchi wake na kuleta maendeleo katika Taifa, usikilizaji na utatuzi wa kero za Wananchi kuanzia Ngazi ya Mtaa mpaka katika Halmashauri zao, kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti Uhalifu, kusimamia usafi wa mazingira ili kuweka Mkoa katika hali ya usafi pamoja na usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nendeni mkatimize wajibu wenu ipasavyo na mkatekeleze matarajio ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo.” amesema RC Sendiga.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael John Semindu ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyoagizwa na mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza majukumu yao yote kwa weledi.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.