Bodi ya Afya Halmashauri ya Mji wa Mbulu imefanya ziara ya siku moja Halmashauri ya Mji wa Babati kujifunza namna bora ya utoaji wa huduma kwa Wananchi ikiwemo wagonjwa wanaopata huduma kwa msamaha pamoja na upatikanaji wa Dawa katika maeneo ya utoaji wa huduma za Afya.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Silvester Ombay ameongoza ziara hiyo akiwa ameambatana na wajumbe wa Bodi, ambapo ametoa pongezi kwa Bodi ya Afya Halmashauri ya Mji wa Babati kwa namna ilivyofanikiwa kutoa huduma bora za Afya kwa Wananchi na kuongeza kuwa watakwenda kuyafanyia kazi mazuri yote waliyoyaona
"Huduma za Usafi na utoaji wa huduma za Afya katika Mji huu zimeturidhisha sana, tunakwenda kuyafanyia kazi na pale tulipokuwa tunaenda kinyuma au taratibu basi tutakwenda kurekebisha ili tuweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wa Mbulu". Alisema Bw.Ombay
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bi. Rehema Bwasi baada ya ziara hiyo amesema bodi imejifunza mambo mengi ya msingi ambayo yatakwenda kubadilisha utoaji wa huduma hiyo katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na kufikia lengo la Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutoa huduma bora kwa kila mwananchi.
"Lengo la Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais ni kuboresha huduma zote muhimu kwa wananchi ikiwemo sekta ya Afya ambayo ndio kipaumbele muhimu zaidi kulinda Afya za Watanzania wakiwemo wana Mbulu, lakini hali ya Mazingira kuwa safi katika mji huu wa Babati wakati wote, hivyo haya tuliyojifunza tunakwenda kuyatekeleza na wataalamu wetu chini ya usimamizi wa bodi hii". Aliongeza Bwasi
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mbulu Ndugu.Paulo Bura amesema kufuatia ziara hiyo muhimu kufanyika leo, Wilaya ya Mbulu itaendelea kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza Mazingira na watalaamu wa Afya kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi pamoja na makundi maalumu wakiwemo Wazee, wanawake na watoto.
Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Dr. Gilliard Lupembe amesema mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa katika utoaji wa huduma zilizo bora katika Mji na Hospitali hiyo ni Watalaamu kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuzingatia Sheria, taratibu za utoaji huduma na utu kwa wagonjwa.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.