Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Mbulu likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Peter Sulle Januari 29, 2025, limepitisha rasimu ya Mpango wa bajeti ya Shilingi Bilioni 28.3 kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, kikao hicho maalumu kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa mbulu.
Akiwasilisha bajeti hiyo kwaniaba ya Mkurugenzi Afisa Mipango Ndugu. Ally Msangi alieleza kuwa mapendekezo ya bajeti yameandaliwa kwa kuzingatia vipaombele ikiwemo Miradi Viporo,Mikopo ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu,masuala mazima ya watumishi na mambo mengine yote yanayohusu Halmashauri kulingana na bajeti.
Kwa niaba ya Waheshimiwa Madiwani wengine akiwemo Diwani wa kata ya Kainam Mhe.Emmanuel Malley, Diwani wa kata ya Imboru Mhe. Basili Gwawu, Diwani wa kata ya Daudi Mhe. Peter Golis na Diwani wa Kata ya Gunyoda Mhe. Juliana Musso wametoa pongezi kwa timu nzima ya wataalamu wa Halmashauri kwa maandalizi ya bajeti ambayo imewagusa miradi ya maendeleo ya wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu kwa asimilia kubwa.
Sambamba na hayo wamesisitiza ushirikiano wa karibu kati ya madiwani na wataalamu ili kuendelea kuimarisha vyanzo vya mapato na kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kufikia malengo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Mhe. Peter Sulle alihitimisha Mkutano huo kwa kuwasisitiza Wataalamu kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo ili kutimiza malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwasogezea wananchi huduma muhimu za kijamii.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.