Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu, Ndugu.Paulo Bura akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael Semindu katika hafla ya uzinduzi wa chanjo ya mifugo uliyofanyika katika kijiji cha Guneneda kata ya Tlawi leo Agosti 28,2025.
Akizungumza katika hafla hiyo Ndugu. Bura amewaeleza wananchi kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha mifugo yote inakuwa na afya njema na inakuwa salama kwa matumizi ya kitoweo kwa binadamu ndiyo maana serikali imeamua kupunguza gharama za chanjo ya mifugo.
Halmashauri ya Mji wa Mbulu inatarajia kutoa chanjo ya mifugo kwa ng’ombe elfu hamsini na nne (54,000),kondoo na mbuzi elfu Hamsini na nne (54,000) Pamoja na kuku laki moja na elfu kumi(110,000).
“Gharama halisi ya chanjo ya ng’ombe ni shilingi elfu moja(1000/=)lakini serikali imepunguza hadi kufikia shilingi mia tano (500/=),gharama halisi kwa mbuzi na kondoo ni shilingi mia sita (600/=) lakini serikali imepunguza hadi kufikia shilingi mia tatu (300/=) kwa kila mfugo na kwa wafugaji wa kuku chanjo itatolewa bure", alisema Ndugu.Bura
Sambamba na hayo ameendelea kuwasisitiza wafugaji kuwa mabalozi kwa wafugaji wote kwa kuwaeleza wafugaji wengine umuhimu wa chanjo kwa mifugo yao ili kutimiza lengo la serikali katika zoezi la utoaji wa chanjo za mifugo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Guneneda Mhe. Christopher Gabriel ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wafugaji na kutoa chanjo ya mifugo kwa ruzuku.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.