Timu ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, ikiongozwa na Katibu Tawala Msaidizi, Ndugu Dominick Mbwete, leo Septemba 24, 2025 imeanza ziara ya siku mbili ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Ndugu Mbwete alisisitiza umuhimu wa shule zote zilizopokea fedha mwishoni mwa mwaka wa fedha 2024/2025 na mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuanza mara moja utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora.
“Ili kutimiza dhamira ya Serikali ya kupeleka fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyopangwa,” alisema Mbwete.
Aidha, aliongeza kusisitiza kuwa miradi yote inayoendelea kutekelezwa lazima izingatie taratibu za kiserikali na kufuata viwango vya ubora vinavyokubalika, ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha za umma inaonekana kwa wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Ndugu Philemon Maffa, ameahidi kwamba Halmashauri ya Mji wa Mbulu, itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya na kufanikisha malengo ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Miradi iliyotembelewa ni miradi inayotarajia kuanza kutekelezwa ikiwemo ukarabati wa shule ya Msingi Daudi,Ujenzi wa madarasa 3,matundu
6 ya vyoo katika Shule ya Msingi Laban na Ujenzi wa madarasa 3 na Matundu 6 ya vyoo katika Shule ya Msingi Ayamohe.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.