Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mazingira Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka Septemba 26, leo Septemba 24, 2025, Afisa Usimamizi wa Taka na Usafi wa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Ndugu Restituta Kadashi, alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi kupitia Redio ya Jamii iitwayo Redio Habari Njema.
Akizungumza kupitia redio hiyo, Ndg. Restituta aliwakumbusha wananchi kuwa lengo kuu la maadhimisho haya ni kuhimiza ushiriki wa jamii katika kuimarisha huduma za afya na kuendeleza usafi wa mazingira.
Alifafanua kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbulu imejipanga kikamilifu kushiriki maadhimisho hayo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kata ya Sanubaray (Mtaa wa Sanu Kati), Kata ya Uhuru (Mtaa wa Harka) na Kata ya Imboru (Mtaa wa Bomani).
“Naomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho haya, hususan kwenye shughuli za usafi wa kaya, maeneo ya biashara, masoko, taasisi, mifereji na sehemu zingine za umma ili kuhakikisha mazingira yanayotuzunguka yanabaki safi,” alisema Ndg. Restituta.
Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mazingira Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Tokomeza Taka za Plastiki, Jenga Jamii Yenye Afya Bora.”
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.