Jeshi la Magereza Wilaya ya Mbulu leo Agosti 23,2025, limeonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa jamii kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo mchele, mahindi, mafuta ya kupikia, sukari, dawa za meno, taulo za kike (pedi) pamoja na baiti za watoto katika Shule ya Msingi Endagkot kwa Watoto Wenye mahitaji maalumu.
Msaada huu umetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 64 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza baada ya Uhuru wa Tanganyika, maadhimisho ambayo kwa mwaka huu yanafanyika kitaifa Ukonga, Jijini Dar es Salaam, yakitarajiwa kuhudhuriwa na Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kama mgeni rasmi.
Mkuu wa Gereza la Mbulu, Sajenti Sp. Raulent Mushi, amesema kuwa Kituo cha Gereza la Mbulu kimeamua kuadhimisha siku hii kwa shughuli mbalimbali ikiwemo jogging ya pamoja, kufanya usafi, pamoja na kutoa zawadi kwa watoto wenye uhitaji maalumu wa Kata ya Endagikoti.
Aidha, amaeongeza kusema lengo kuu la shughuli hizo ni kuonesha mshikamano na jamii na pia kuthibitisha kuwa maadhimisho ya Jeshi la Magereza ni tukio la kitaifa linaloleta mshikikano na matendo ya huruma kila mahali.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Endagikot na Msimamizi wa Watoto, Ndugu Costansia Joseph Pissa, ameishukuru Jeshi la Magereza Mbulu kwa msaada wa chakula walichowapatia watoto.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za chakula cha mchana kwa watoto hao.
Hata hivyo, mpaka sasa kituo kina jumla ya watoto 56 wakiwemo wavulana 32 na wasichana 22. Imeelezwa kuwa kituo hicho kina bweni la wasichana pekee, huku watoto wote wakiendelea kuwa na mahitaji mbalimbali ya msingi.
Nae kaimu mkuu wa Idara ya Elimu Msingi , Ndugu. Zakaria Nyinyimbe ametoa shukrani kwa Jeshi la Magereza kwa kuona umuhimu wa kushirikiana katika kuwalea watoto. Amesema kitendo kilichofanyika ni kielelezo cha uzalendo na utu.
“Ujumbe huu utaifikia jamii na wadau wa elimu, ambao nao wataona wajibu wao wa kuchangia malezi ya watoto. Vilevile, watoto wenyewe wameona mfano huu na watapata fursa ya kujifunza kutoka kwake. Mungu awatie nguvu, na tunawakaribisha kwa moyo wa dhati kila wakati.”
Miongoni mwa wanafunzi wenye Mahitaji maalumu Birigita Daniel ametoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake kwa msaada uliotolewa na Jeshi la Magereza.
“Tunawakaribisha, tunawashukuru sana kwa kutuletea zawadi hizi. Mungu awazidishie mlipotoa”.Alisema Birigita
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.