
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, amewataka watendaji wa kata, vijiji na mitaa pamoja na wataalamu wa sekta mbalimbali kushiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa watoto kuripoti shuleni, pamoja na kuchukua hatua madhubuti kudhibiti utoro ili kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao ya elimu.
Akitoa rai hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichoketi kujadili na kupitia mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa usimamizi thabiti wa elimu unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya viongozi, wataalamu, wazazi na jamii kwa ujumla.
Alieleza kuwa juhudi za kuongeza mahudhurio shuleni zinapaswa kwenda sambamba na mikakati ya kuboresha mazingira ya kujifunzia, ikiwemo kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni na kuimarisha ufuatiliaji wa wanafunzi wanaokosa masomo mara kwa mara.
Katika kikao hicho, wajumbe walijadili kwa kina mapendekezo ya mpango na bajeti, ⁶wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha rasilimali za wilaya zinapangwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi na kuimarisha huduma za msingi kama elimu, afya, maji na miundombinu.
Aidha, wajumbe walikubaliana kuongeza juhudi za uhamasishaji kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu na kuwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanahudhuria shule bila kukosa, huku wakisisitiza ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa.
Kikao kilihitimishwa kwa maazimio ya kuendelea kuboresha mapendekezo ya mpango na bajeti kabla ya kuwasilishwa katika hatua zinazofuata, kwa lengo la kuhakikisha mipango ya maendeleo ya Wilaya ya Mbulu inaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.