



Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu mkoani Manyara wamepitisha kwa kishindo bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Shilingi bilioni 33.2 katika Baraza Maalum la Madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Mhe. Sylvester Ombay, amesema bajeti hiyo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi na imezingatia mahitaji halisi ya Halmashauri.
“Bajeti hii imepitia kamati zote, imejadiliwa na kuboreshwa. Ni wajibu wetu kuipitisha ili ilete maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema Mhe. Ombay.
Diwani wa Kata ya Gehandu, Mhe. Alexander Tango, amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa ushirikishwaji wa madiwani wote na kuwataka wajumbe kuipitisha kwa maslahi ya wananchi.
Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Ndugu Gerald Makombe, amesema Halmashauri inatarajia kutumia kiasi hicho cha Shilingi bilioni 33.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.5 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/2026.
Kwa mujibu wa Ndugu Makombe, katika mchanganuo wa bajeti hiyo, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 3.2 huku asilimia 40% zikilenga kutekeleza miradi ya maendeleo.
Baada ya majadiliano, madiwani kwa pamoja walieleza kuridhishwa na bajeti hiyo, wakisisitiza kuwa imejikita katika kutatua changamoto za wananchi na kuharakisha maendeleo ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Copyright ©2020 GWF . All rights reserved.